Ezekieli 21:1-17
Ezekieli 21:1-17 SRUV
Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, uelekeze uso wako Yerusalemu, ukadondoze neno lako upande wa mahali patakatifu, ukatabiri juu ya nchi ya Israeli; uiambie nchi ya Israeli, BWANA asema hivi; Tazama, mimi ni juu yako, nami nitautoa upanga wangu alani, nami nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mbaya. Basi, kwa kuwa nitamkatilia mbali nawe mtu mwenye haki na mtu mwovu, upanga wangu utatoka alani mwake, uwe juu ya watu wote wenye mwili toka kusini hadi kaskazini, na watu wote wenye mwili watajua ya kuwa mimi, BWANA, nimeufuta upanga wangu alani mwake; hautarudi tena. Piga kite, basi, Ee mwanadamu; kwa kuvunjika moyo na uchungu mwingi mbele ya macho yao. Na itakuwa, wakuambiapo, Mbona unapiga kite? Ndipo utakaposema, Kwa sababu ya habari hizo, maana linakuja; na kila moyo utayeyuka, na mikono yote itakuwa dhaifu, na kila roho itazimia, na magoti yote yatageuka kuwa kama maji; tazama, linakuja, nalo litatendeka, asema Bwana MUNGU. Neno la BWANA likanijia, kusema, Mwanadamu, tabiri, useme, BWANA asema hivi; Nena, Upanga, upanga, umenolewa na kusuguliwa, umenolewa ili kufanya machinjo; umesuguliwa ili uwe kama umeme; basi je! Tufanye furaha? Upanga unadharau fimbo ya mwanangu, kama unavyodharau kila mti. Nao umetolewa ili ung'arishwe upate kushikwa mkononi; upanga umenolewa, naam, umesuguliwa, ili kutiwa katika mkono wake auaye. Piga kelele, utoe sauti ya uchungu, Ee mwanadamu, kwa maana upanga u juu ya watu wangu, u juu ya wakuu wote wa Israeli; wametolewa wauawe na upanga pamoja na watu wangu, basi, jipige pajani. Kwa maana kuna kujaribiwa; itakuwaje, basi, ikiwa upanga unaidharau hiyo fimbo? Haitakuwapo tena; asema Bwana MUNGU. Basi, wewe mwanadamu, tabiri, ukapige makofi; upanga huo na uongezwe mara mbili, hata mara tatu; upanga wao waliotiwa jeraha kiasi cha kuwaua; ni upanga wa mkuu aliyetiwa jeraha kiasi cha kumwua; uwazungukao pande zote. Nimeweka ncha ya upanga huo juu ya malango yao yote, ili mioyo yao iyeyuke, yakaongezeke makwazo yao; aha! Umefanywa kuwa kama umeme, umenolewa, ili uchinje. Jiweke tayari, nenda upande wa kulia; jipange, nenda upande wa kushoto; mahali popote utakapouelekeza uso wako. Mimi nami nitapiga makofi, mimi nami nitashibisha ghadhabu yangu; mimi, BWANA, nimenena neno hili.