Ezekieli 21:1-17
Ezekieli 21:1-17 BHN
Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, ugeukie mji wa Yerusalemu, uhubiri dhidi ya sehemu zake za ibada, na kutoa unabii juu ya nchi ya Israeli. Waambie Waisraeli kuwa mimi Mwenyezi-Mungu nasema hivi: Mimi mwenyewe naja kupambana nanyi. Nitauchomoa upanga wangu alani mwake na kuwaua watu wema na wabaya. Tangu kaskazini hadi kusini, nitawakatilia mbali watu wote, wema na wabaya, kwa upanga wangu. Watu wote watajua kuwa mimi Mwenyezi-Mungu ndiye niliyeuchomoa upanga alani mwake na wala hautarudishwa tena ndani. “Nawe mtu, jikunje kama mtu aliyekata tamaa, uomboleze mbele yao. Wakikuuliza, ‘Kwa nini unaomboleza?’ Utawaambia: ‘Naomboleza kwa sababu ya habari zinazokuja.’ Kila mtu atakufa moyo, mikono yao yote italegea; kila aishiye atazimia na magoti yao yatakuwa kama maji. Habari hizo zaja kweli, nazo zinatekelezwa. Mimi Bwana Mwenyezi-Mungu nimesema.” Neno la Mwenyezi-Mungu lilinijia: “Wewe mtu, toa unabii useme: Mwenyezi-Mungu asema hivi: Upanga! Naam, upanga umenolewa, nao umengarishwa pia. Umenolewa ili ufanye mauaji, umengarishwa umetamete kama umeme! Umenolewa na kungarishwa uwekwe mkononi mwa mwuaji. Wewe mtu, lia na kuomboleza upanga huo umenyoshwa dhidi ya watu wangu, dhidi ya wakuu wote wa Israeli. Wataangamizwa kwa upanga pamoja na watu wangu. Jipige kifua kwa huzuni. Hilo litakuwa jaribio gumu sana. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema. Wewe mtu, tabiri! Piga makofi, upanga na ufanye kazi yake, mara mbili, mara tatu. Huo ni upanga wa mauaji nao unawazunguka. Kwa hiyo wamekufa moyo na wengi wanaanguka. Ncha ya upanga nimeiweka katika malango yao yote. Umefanywa ungae kama umeme, umengarishwa kwa ajili ya mauaji. Ewe upanga, shambulia kulia, shambulia kushoto; elekeza ncha yako pande zote. Nami nitapiga makofi, nitatosheleza ghadhabu yangu. Mimi Mwenyezi-Mungu nimesema.”