Ayubu 22:1-11
Ayubu 22:1-11 NEN
Ndipo Elifazi Mtemani akajibu: “Je, mwanadamu aweza kuwa wa faida kwa Mungu? Je, hata mtu mwenye hekima aweza kumfaidi? Je, Mwenyezi angefurahia nini kama ungekuwa mwadilifu? Au je, yeye angepata faida gani kama njia zako zingekuwa kamilifu? “Je, ni kwa ajili ya utaua wako ndiyo maana anakukemea na kuleta mashtaka dhidi yako? Je, uovu wako si mkuu? Dhambi zako si hazina mwisho? Umedai dhamana kwa ndugu zako bila sababu; umewavua watu nguo zao, ukawaacha uchi. Hukumpa maji aliyechoka, nawe ulimnyima chakula mwenye njaa, ingawa ulikuwa mtu mwenye uwezo ukimiliki nchi: mtu uliyeheshimiwa, ukiishi ndani yake. Umewafukuza wajane mikono mitupu na kuzivunja nguvu za yatima. Ndiyo sababu mitego imekuzunguka pande zote, hatari ya ghafula inakutia hofu, ndiyo sababu ni giza sana huwezi kuona, tena ndiyo sababu mafuriko ya maji yamekufunika.