Yobu 22:1-11
Yobu 22:1-11 BHN
Kisha Elifazi, Mtemani, akajibu Yobu: “Je, binadamu anafaa chochote kwa Mungu? Kwa kweli mwenye hekima anajifaidi mwenyewe tu. Je, unadhani wamfurahisha Mungu kwa kuwa mnyofu? Au anapata faida gani kama huna hatia? Unadhani anakurudi na kukuhukumu kwa sababu wewe unamheshimu? La! Uovu wako ni mkubwa mno! Ubaya wako hauna mwisho! Wewe umemnyanganya ndugu yako nguo ya rehani; umemchukulia nguo hiyo moja aliyokuwa nayo. Umewanyima maji wale waliokuwa wamechoka; umewanyima chakula wale walio na njaa. Umemruhusu mwenye cheo kuchukua ardhi yote; umemwacha anayependelewa aishi humo. Umewaacha wajane waende mikono mitupu; umewanyima yatima uwezo wao. Kwa hiyo mitego imekuzunguka pande zote, hofu ya ghafla imekuvamia. Giza limekuangukia usione kitu; mafuriko ya maji yamekufunika.