Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

Mithali 25:18-28

Mithali 25:18-28 NEN

Kama vile rungu au upanga au mshale mkali ndivyo alivyo mtu atoaye ushuhuda wa uongo dhidi ya jirani yake. Kama vile jino bovu au mguu uliolemaa, ndivyo ilivyo kumtegemea mtu asiye mwaminifu wakati wa shida. Kama vile avuaye mavazi siku ya baridi, au kama siki iliyomwagwa juu ya magadi, ndivyo alivyo yeye amuimbiaye nyimbo mtu mwenye moyo mzito. Kama adui yako ana njaa, mpe chakula ale; kama ana kiu, mpe maji anywe. Kwa kufanya hivyo, unaweka makaa ya moto yanayowaka kichwani pake, naye BWANA atakupa thawabu. Kama vile upepo wa kaskazini uletavyo mvua, ndivyo ulimi usingiziao uletavyo uso wa hasira. Ni afadhali kuishi pembeni mwa paa la nyumba, kuliko kuishi nyumba moja na mke mgomvi. Kama vile maji baridi kwa nafsi iliyochoka ndivyo zilivyo habari njema kutoka nchi ya mbali. Kama vile chemchemi iliyotibuliwa matope au kisima kilichotiwa taka ndivyo alivyo mtu mwenye haki akishiriki na waovu. Si vyema kula asali nyingi sana, wala si heshima kujitafutia heshima yako mwenyewe. Kama vile mji ambao kuta zake zimebomoka ndivyo alivyo mtu ambaye hawezi kujitawala mwenyewe.

Mipango ya Kusoma Bila Malipo na Ibada zinazohusiana na Mithali 25:18-28