Methali 25:18-28
Methali 25:18-28 BHN
Mtu atoaye ushahidi wa uongo dhidi ya mwenziwe, ni hatari kama rungu, upanga au mshale mkali. Kumtegemea mtu asiyeaminika wakati wa taabu, ni kama jino bovu au mguu ulioteguka. Kumwimbia mtu mwenye huzuni, ni kama kuvua nguo wakati wa baridi, au kutia siki katika kidonda. Adui yako akiwa na njaa, mpe chakula; akiwa na kiu, mpe maji ya kunywa. Hivyo utafanya apate aibu kali, kama makaa ya moto kichwani pake, naye Mwenyezi-Mungu atakutuza. Upepo wa kusi huleta mvua, hali kadhalika masengenyo huleta chuki. Afadhali kuishi pembeni juu ya paa, kuliko kuishi nyumbani pamoja na mwanamke mgomvi. Kama vile maji baridi kwa mwenye kiu, ndivyo habari njema kutoka mbali. Mwadilifu akubaliye kufuata mambo ya mwovu, ni chemchemi iliyochafuliwa au kisima kilichotibuliwa. Si vizuri kula asali nyingi mno; kadhalika haifai kujipendekeza mno. Mtu asiyeweza kuzuia hasira yake, ni kama mji usio na ulinzi unaposhambuliwa.