Mwa 18:1-15
Mwa 18:1-15 SUV
BWANA akamtokea Ibrahimu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa hari. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka nchi, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, iwapo mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Ibrahimu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Himiza vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Ibrahimu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng’ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akahimiza kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandikia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Ibrahimu na Sara walikuwa wazee, na umri wao mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Ibrahimu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo, umecheka.