Mwanzo 18:1-15
Mwanzo 18:1-15 SRUV
BWANA akamtokea Abrahamu karibu na mialoni ya Mamre, alipokuwa ameketi mlangoni pa hema yake mchana wakati wa joto. Akainua macho yake akaona, na tazama, watu watatu wamesimama mbele yake. Naye alipowaona alipiga mbio kuwalaki kutoka mlangoni pa hema, akainama mpaka chini, akasema, Bwana wangu, kama nimeona fadhili machoni pako nakuomba usinipite sasa mimi mtumwa wako. Na yaletwe basi maji kidogo mkanawe miguu, mkapumzike chini ya mti huu. Nami nitaleta chakula kidogo, mkaburudishe moyo, baadaye mwendelee, kwa maana mmemjia mtumwa wenu. Wakasema, Haya, fanya kama ulivyosema. Basi Abrahamu akaenda hima hemani kwa Sara, akasema, Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga safi, uukande, ufanye mikate. Abrahamu akapiga mbio kwenda kundini, akaleta ndama wa ng'ombe aliye laini, mzuri, akampa mtumishi, naye akaharakisha kuiandaa. Akatwaa siagi na maziwa, na ndama aliyoiandaa, akawaandalia mbele yao, akasimama karibu nao chini ya mti, nao wakala. Wakamwambia, Yu wapi Sara mkeo? Akasema, Yumo hemani. Akamwambia, Hakika nitakurudia wakati huu huu mwakani, na tazama, Sara mkeo atapata mwana wa kiume. Sara akasikia mlangoni pa hema iliyokuwapo nyuma yake. Basi Abrahamu na Sara walikuwa wazee wenye umri mkubwa, na Sara alikuwa amekoma katika desturi ya wanawake. Kwa hiyo Sara akacheka moyoni mwake, akisema, Niwapo mkongwe, nitapata furaha, na bwana wangu mzee? BWANA akamwambia Abrahamu, Mbona Sara amecheka akisema, Mimi kweli nitazaa mwana, nami ni mzee? Kuna neno gani lililo gumu la kumshinda BWANA? Kwa muhula wake nitakurudia, wakati huu huu mwakani, na Sara atapata mwana wa kiume. Akakana Sara, akisema, Sikucheka, maana aliogopa. Naye akasema, Sivyo! Umecheka.