Mwanzo 18:1-15
Mwanzo 18:1-15 BHN
Mwenyezi-Mungu alimtokea Abrahamu penye mialoni ya Mamre. Abrahamu alikuwa ameketi penye mlango wa hema lake wakati wa joto la mchana, na alipoinua macho yake, akaona watu watatu wamesimama mbali kidogo mbele yake. Mara alipowaona, akapiga mbio kutoka mlangoni mwa hema lake, akaenda kuwalaki. Alipowafikia aliinama kwa heshima na kusema, “Bwana zangu, kama mnanipenda tafadhali msinipite mimi mtumishi wenu ila mshinde kwangu. Mtaletewa maji kidogo ili mnawe miguu na kupumzika chini ya mti. Wakati mnapopumzika, nitaandaa chakula kidogo, mle, ili mpate nguvu za kuendelea na safari yenu; maana mmenijia mimi mtumishi wenu.” Nao wakasema, “Sawa! Fanya kama ulivyosema.” Abrahamu akarudi haraka hemani akamwambia Sara, “Tayarisha haraka vipimo vitatu vya unga bora, uukande, uoke mikate.” Kisha akatoka haraka akaenda kwenye kundi la ng'ombe, akachagua ndama mmoja mzuri na mnono, akamkabidhi mtumishi ambaye aliharakisha kumchinja na kumpika. Halafu Abrahamu akachukua siagi, maziwa na ile nyama iliyotayarishwa, akawaandalia wageni hao chakula; naye akasimama karibu nao kuwahudumia walipokuwa wakila chini ya mti. Wale wageni wakamwuliza, “Mkeo Sara yuko wapi?” Abrahamu akawajibu, “Yumo hemani.” Mmoja wao akasema, “Hakika nitakurudia wakati kama huu mwakani, na mkeo Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Sara alikuwa huko nyuma mlangoni mwa hema, akisikiliza. Abrahamu na Sara walikuwa wakongwe, naye Sara mambo ya kawaida ya wanawake yalikuwa yamekoma kitambo. Kwa hiyo, Sara alicheka kimoyomoyo akisema, “Mimi ni mzee, na mume wangu hali kadhalika. Je, nikiwa mzee hivi, nitaweza kufurahi na kupata watoto?” Hapo Mwenyezi-Mungu akamwuliza Abrahamu, “Kwa nini Sara amecheka na kujiuliza kama kweli itawezekana apate mtoto akiwa mzee? Je, kuna jambo lolote lisilowezekana kwa Mwenyezi-Mungu? Nitakurudia wakati uliopangwa, wakati kama huu mwakani, na Sara atakuwa na mtoto wa kiume.” Lakini Sara, akiwa na hofu, akakana akisema, “Sikucheka!” Mwenyezi-Mungu akamwambia, “Sivyo! Kucheka, ulicheka.”