Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Mose 47

47
Waisiraeli wanakalishwa Goseni.
1Kisha Yosefu akaingia kwake Farao, akampasha habari kwamba: Baba yangu na ndugu zangu na mbuzi na kondoo wao na ng'ombe wao pamoja nayo yote, waliyokuwa nayo, wametoka katika nchi ya Kanaani, sasa wako katika nchi ya Goseni. 2Alikuwa amewachukua ndugu zake watano waliozaliwa wa mwisho kuwasimamisha mbele ya Farao. 3Farao alipowauliza: Kazi yenu nini? wakamwambia Farao: Watumwa wako ni wachungaji; nasi tulivyo, ndivyo, nao baba zetu walivyokuwa.#1 Mose 46:33-34. 4Tena wakamwambia Farao: Tumekuja kukaa ugenini katika nchi hii, kwani mbuzi na kondoo wao watumwa wako hawana malisho, kwani njaa ni nzito katika nchi ya Kanaani; sasa acha, watumwa wako wakae katika nchi ya Goseni! 5Ndipo, Farao alipomwambia Yosefu kwamba: Baba yako na ndugu zako wamekuja kwako. 6Basi, nchi ya Misri iko wazi machoi pako; mkalishe baba yako pamoja na ndugu zako katika nchi iliyo nzuri zaidi! Na wakae katika nchi ya Goseni! Nao, uwajuao kuwa mafundi wa kazi hiyo, uwaweke kuwa wakuu wao wanaoyachunga makundi yangu.
Yakobo anaonana na Farao.
7Kisha Yosefu akampeleka baba yake Yakobo, akamsimamisha mbele ya Farao, naye Yakobo akambariki Farao. 8Farao alimpomwuliza Yakobo: Miaka yako ya kuwapo ni mingapi? 9Yakobo akamjibu Farao: Siku za miaka ya kukaa huku ugenini ni miaka 130. Siku za miaka ya maisha yangu ni chache, tena ni mbaya, hazikufika kuwa nyingi kama siku za miaka ya kuwapo za baba zangu, walizozikaa huku ugenini.#Sh. 90:10; 36:12. 10Yakobo akambariki Farao, kisha akatoka mwake Farao.
11Yosefu akampatia baba yake na ndugu zake mahali pa kukaa, akawapa kipande cha nchi ya Misri, wakichukue, nacho kilikuwa nchi nzuri zaidi katika nchi ya Ramusesi, kama Farao alivyoagiza. 12Yosefu akamtunza baba yake na ndugu zake nao wote wa mlango wa baba yake akiwapa chakula kwa hesabu ya watoto wao.#1 Mose 45:11.
Njaa inazidi huko Misri.
13Chakula hakikuwako katika nchi zote, kwa kuwa njaa ilikuwa nzito sana, nayo nchi ya Misri nayo nchi ya Kanaani zikaenda kuzimia kwa ajili ya njaa. 14Yosefu akazikusanya fedha zote zilizopatikana katika nchi ya Misri na katika nchi ya Kanaani kwa kuuza ngano, watu walizozinunua; naye Yosefu akazipeleka hizo fedha nyumbani mwake Farao. 15Fedha zilipotoweka katika nchi ya Misri, Wamisri wote wakaja kwa Yosefu, wakamwambia: Tupe chakula! Mbona tufe machoni pako, kwa kuwa hatuna fedha? 16Naye Yosefu akasema: Leteni nyama, kama hamna fedha! 17Ndipo, walipopeleka kwa Yosefu nyama, waliowafuga, naye Yosefu akawapa chakula kwa farasi wao na kwa makundi yao ya mbuzi na kondoo na kwa makundi yao ya ng'ombe na kwa punda wao; ndivyo, alivyowatunza mwaka huo na kuwapa chakula kwa makundi yao yote.
18Mwaka huo ulipokwisha, wakaja kwake nao mwaka wa pili, wakamwambia: Hatutaki kumficha bwana wetu, ya kama fedha zimekwisha, nayo makundi ya nyama, tuliowafuga, wamekwenda kwa bwana wetu, hakuna yetu tena yaliyosalia mbele ya bwana wetu, isipokuwa miili yetu na mashamba yetu. 19Mbona tufe machoni pako sisi na mashamba yetu? Tununue sisi na mashamba yetu kwa chakula, sisi na mashamba yetu tuwe mali zake Farao! Tena tupe mbegu, tusife, nayo mashamba yasiwe mapori matupu! 20Ndivyo, Yosefu alivyomnunulia Farao mashamba yote ya Misri, kwani Wamisri waliuza kila mtu shamba lake, kwani njaa ilikuwa kali kwao; ndivyo, hiyo nchi ilivyopata kuwa yake Farao mwenyewe. 21Nao watu akawahamisha kukaa mijini toka mpaka wa kwanza wa Misri hata mpaka wake wa mwisho. 22Mashamba ya watambikaji tu hakuyanunua, kwani hao watambikaji walikatiwa hayo mashamba na Farao kuwa chakula chao, nao wakajitunza na kuitumia hiyo haki, Farao aliyowapa; kwa sababu hii hawakuyauza mashamba yao.
23Kisha Yosefu akawaambia watu: Tazameni, nimewanunua leo ninyi na mashamba yenu kuwa mali zake Farao; ninawapa hapa mbegu za kupanda katika mashamba yenu. 24Hapo, mtakapovuna, sharti mmpe Farao fungu la tano! Mafungu manne yatakuwa yenu ya kupanda mashambani na ya kula ninyi nao waliomo manyumbani mwenu na watoto wenu. 25Ndipo, waliposema: Umetuponya. Tumeona mapendeleo machoni pa bwana wetu, na tuwe watumwa wake Farao! 26Hayo maongozi, Yosefu aliyoyaweka, yako mpaka siku hii ya leo kwamba: Fungu la tano la mapato ya mashamba ya Misri ni lake Farao. Mashamba yasiyouzwa kuwa yake Farao ni yale ya watambikaji peke yao tu.
Kufa kwake Yakobo kunafika karibu.
27Ndivyo, Waisiraeli walivyokaa huko Misri katika nchi ya Goseni, wakaichukua kuwa yao, wakazaa wana, wakawa wengi sana.#1 Mose 46:3; 2 Mose 1:7,12. 28Yakobo akawapo katika nchi ya Misri miaka 17; hivyo siku za miaka ya maisha yake Yakobo zikawa miaka 147. 29Siku za kufa kwake Isiraeli zilipofika karibu, akamwita mwanawe Yosefu, akamwambia: Kama nimeona upendeleo machoni pako, uweke mkono wako chini ya kiuno changu, unifanyizie wema na welekevu huu, usinizike huku Misri,#1 Mose 24:2. 30nipate kulala kwa baba zangu. Kwa hiyo unichukue na kunitoa huku Misri, upate kunizika kaburini mwao! Naye akasema: Nitafanya, kama ulivyosema.#1 Mose 25:9,10; 49:29-32. 31Aliposema: Uniapie! akamwapia. Kisha Isiraeli akauinamia upande wa kichwani wa kitanda na kusali.

Iliyochaguliwa sasa

1 Mose 47: SRB37

Kuonyesha

Shirikisha

Nakili

None

Je, ungependa vivutio vyako vihifadhiwe kwenye vifaa vyako vyote? Jisajili au ingia