BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaMfano
Yesu anawafunza wafuasi wake waepuke unafiki wa viongozi wa dini. Wanazungumza kuhusu upendo wa Mungu lakini wanawapuuza maskini. Wanafahamu mengi sana lakini wanatumia ufahamu wao kupata sifa. Yesu analaani maisha haya vuguvugu na anafundisha kuwa Mungu anaona yote na kila mtu atatoa hesabu yake. Hili ni onyo na pia ni himizo. Ni onyo kwa sababu tamaa na masengenyo hatimaye yatafichuliwa. Wanafiki watajulikana. Ukweli utafunuliwa na maovu yatarekebishwa siku moja. Lakini pia ni himizo sababu Mungu haoni tu uovu wa wanadamu; anaona mema pia. Anaona mahitaji ya wanadamu na anajali viumbe wake. Yesu anawahakikishia wafuasi wake kuwa wakiutafuta Ufalme wa Mungu na kuutanguliza, watapokea hazina ya milele na yote wanayohitaji ulimwenguni. Bila shaka, hii haimaanishi kuwa maisha yatakuwa rahisi. Kwa hakika, Yesu anakubali kwamba wafuasi wake watapitia mateso. Lakini anaahidi kuwa watakaopitia mateso watamwona Mungu, na wanaoyatoa maisha yao ili kulitukuza jina lake watatukuzwa mbele za malaika. Kwa sababu hii, Yesu anawahimiza wafuasi wake kuamini kuwa Mungu atawapa mahitaji yao na anawaonya dhidi ya unafiki. Yesu ana tamanio la watu wote kupokea mafundisho yake, lakini wengi wanayakataa.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
•Baada ya kusoma mafundisho ya Yesu leo, unawezaje kufafanua unafiki? Yesu anafananisha unafiki na chachu (12:1). Je, unafiki ni sawa na chachu kivipi?
•Tamaa sio tu hamu ya kupata pesa na mali nyingi. Yesu anatoa mwito kwa wafuasi wake kulinda maisha yao dhidi ya aina zote za tamaa. Je, aina tofauti za tamaa ni zipi? Kwa mfano, fikiria kuwa na tamaa ya kujionyesha, kukubalika au burudani. •Soma Luka 12:29-34. Unatambua nini? Je, wewe hutumia muda wako mwingi kufanya na kuwaza nini? Je, mafundisho ya Yesu yanakuonya au kukuhimiza vipi leo?
•Yesu anafundisha ili kuwalinda watu wake jinsi kuku avikusanyavyo vifaranga vyake chini ya mbawa zake dhidi ya wanyama wawindaji (soma 13:34). Lakini wengi bado hawako radhi kupokea ulinzi wake. Fikiria kuhusu tukio katika maisha yako ambapo ulijutia kutosikiza onyo. Je, ungerudi wakati huo ungejieleza nini?
•Kusoma na kutafakari kwako kukuchochee kuomba. Mshukuru kwa kukulinda dhidi ya tamaa na unafiki, mweleze udhaifu wako na umwombe unachohitaji ili uweze kumfuata leo.
Kuhusu Mpango huu
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More
Tungependa kushukuru shirika la BibleProject kwa kutoa mwongozo huu. Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea: www.bibleproject.com