BibleProject | Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio / Sehemu ya 1 - LukaMfano
Katika sehemu hii ya kitabu cha Luka, Yesu amefikia mwisho wa safari yake ndefu kwenda Yerusalemu. Anawasili akiwa amebebwa kwenye punda kutoka Mlima wa Mizeituni kuelekea mjini. Njiani, umati unamkaribisha kama mfalme huku wakiimba, “Atukuzwe Mfalme ajaye kwa jina la Bwana.” Umati ulikumbuka kuwa manabii wa zamani wa Israeli walitabiri kuwa siku moja Mungu mwenyewe atawasili kuwakomboa watu wake na kutawala ulimwengu. Nabii Zakaria alitabiri kuhusu Mfalme atakayekuja na ataingia Yerusalemu akimwendesha punda ili kuleta haki na amani. Umati unaimba kwa sababu unatambua kuwa Yesu ndiye ameleta matumaini haya yote.
Lakini sio watu wote wanakubali. Viongozi wa kidini wanachukulia utawala wa Yesu kuwa tishio kwa mamlaka yao na wanatafuta njia za kumshtaki na kumkamatisha kwa watawala. Yesu anafahamu yatakayotokea. Anajua kuwa Israeli haitamkubali kama Mfalme na kuwa kukataa kwao kutawaelekeza kwenye njia ya mauti na wataishia kuangamia. Hii inamfadhaisha. Na...inamghadhabisha. Anapoingia Yerusalemu, anaelekea hekaluni na kuwafukuza wafanya biashara wanaozuia utoaji dhabihu. Anasimama katikati ya hekalu na anawaambia, “hii ni nyumba ya sala, lakini mmeifanya kuwa pango la wanyang'anyi.” Hapa anamnukuu nabii Yeremia, aliyesimama palepale, kituo kikuu cha dini na mamlaka ya kisiasa ya Israeli, na akawakosoa viongozi wa kale wa Israeli kwa njia ile ile.
Viongozi wa dini wanaelewa anachosema Yesu, lakini hawakubali na hawajifunzi kutoka kwenye maonyo hayo. Na kama viongozi wa kale wa Israeli waliopanga njama ya kumwangamiza Yeremia, nao pia wanapanga kumwangamiza Yesu. Ili kusimulia tabia ya viongozi wa Israeli, Yesu anaelezea mfano unaomhusu mmiliki wa shamba la mizabibu aliyelikodisha kisha akasafiri. Mmiliki anatuma watumishi kwenye shamba lake la mizabibu ili kuangalia mazao, lakini wakodishaji wanawapiga watumishi wale na kuwafukuza mikono mitupu. Kwa hivyo mmiliki anamtuma mwanawe kwenye shamba lake la mizabibu kwa matumaini kuwa watamheshimu, lakini wakodishaji wanaiona kama fursa ya kujinyakulia shamba lile la mizabibu kwa kumwangamiza mrithi. Wanamfukuza na kumuua. Katika simulizi hii, Yesu analinganisha wapangaji waovu wa shamba lile la mizabibu na viongozi wa kidini wa Israeli ambao mara kwa mara huwakataa manabii wote waliotumwa na Mungu. Nasasa wanajiandaa kumuua mwana mpendwa wa Mungu. Yesu anafafanua kuwa viongozi wa kidini wanatenda makosa yaliyotendwa na baba zao na kuwa hamu na tamaa yao ya kupata mamlaka itawapelekea kuangamia.
Soma, Tafakari, kisha Ujibu:
•Soma Zakaria 9:9-10 na ulinganishe na jinsi Yesu alivyoingia Yerusalemu akiwa amebebwa kwenye punda. Unaona nini?
•Soma Yeremia 7:1-11 na ulinganishe na maandiko ya leo kwenye kitabu cha Luka. Unatambua nini?
•Baada ya kusoma kitabu cha Luka, eleza na ulinganishe mienendo ya wanafunzi wa Yesu na ile ya viongozi wa dini. Je, mienendo hii inakuwezeshaje kujitathmini na kujikosoa? Je, unampokea Yesu vipi leo?
•Kusoma na kutafakari kwako kukuchochee kuomba. Nena na Mungu kuhusu ukuu wake, kiri kuhusu mienendo yako iliyo sawa na ya viongozi wa dini, na umwombe akusaidie uweze kumheshimu kama Mfalme wa maisha yako.
Kuhusu Mpango huu
Shirika la BibleProject liliandaa mwongozo wa Ufalme Unaoenda Kinyume na Matarijio Sehemu ya 1 kuwahimiza watu binafsi, vikundi vidogo na familia kusoma kitabu chote cha Luka kwa siku 20. Mwongozo huu unajumuisha video za katuni, muhtasari wa uchambuzi na maswali ya kutafakari ili kuwasaidia wahusika kumfahamu Yesu na kufuatilia mtiririko wa mawazo ya Luka pamoja na kuyaelewa mafunzo yake.
More
Tungependa kushukuru shirika la BibleProject kwa kutoa mwongozo huu. Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea: www.bibleproject.com