Soma Biblia Kila Siku 09/2025Mfano

Kuenea na kukua kwa Ukristo huambatana na mateso. Mara nyingine mateso haya yanasababisha hata vifo vya Wakristo waliosimama imara kumshudia Kristo kwa wazi. Kwa mfano imeandikwa kuhusu Stefano kwambaakijaa neema na uwezo, alikuwa akifanya maajabu na ishara kubwa katika watu. Lakini baadhi ya watu wa sinagogi lililoitwa sinagogi la Mahuru, na la Wakirene, na la Waiskanderia, na la wale wa Kilikia na Asia, wakaondoka na kujadiliana na Stefano; lakini hawakuweza kushindana na hiyo hekima na huyo Roho aliyesema naye. Hata wakashawishi watu waliosema, Tumemsikia mtu huyu akinena maneno ya kumtukana Musa na Mungu. Wakawataharakisha watu na wazee na waandishi, wakamwendea, wakamkamata, wakampeleka mbele ya baraza. Wakasimamisha mashahidi wa uongo waliosema, Mtu huyu haachi kusema maneno ya kufuru juu ya mahali hapa patakatifu na juu ya torati; maana tumemsikia akisema kwamba Yesu huyo Mnazareti atapaharibu mahali hapa, na kuzibadili desturi tulizopewa na Musa. Watu wote walioketi katika ile baraza wakamkazia macho yao, wakamwona uso wake kuwa kama uso wa malaika(Mdo 6:8-15). Na habari zake zinaendelea hivi katika 7:54-60:Waliposikia maneno haya, wakachomwa mioyo, wakamsagia meno. Lakini yeye akijaa Roho Mtakatifu, akakaza macho yake, akitazama mbinguni, akauona utukufu wa Mungu, na Yesu akisimama upande wa mkono wa kuume wa Mungu. Akasema, Tazama! Naona mbingu zimefunguka, na Mwana wa Adamu amesimama mkono wa kuume wa Mungu. Wakapiga kelele kwa sauti kuu, wakaziba masikio yao, wakamrukia kwa nia moja, wakamtoa nje ya mji, wakampiga kwa mawe. Nao mashahidi wakaweka nguo zao miguuni pa kijana mmoja aliyeitwa Sauli. Wakampiga kwa mawe Stefano, naye akiomba, akisema, Bwana Yesu, pokea roho yangu. Akapiga magoti, akalia kwa sauti kuu, Bwana, usiwahesabie dhambi hii.Akiisha kusema haya akalala. Na Sauli alikuwa akiona vema kwa kuuawa kwake. Tunapokabiliana na matatizo katika maisha ya ufuasi, tusikate tamaa wala kurudi nyuma. Matatizo hayo yapo kwa sababu ya Yesu tunayeongozana naye, na ushindi upo kwa kuwa kazi ya Mungu haishindwi. Anaweza kuyatumia hayo yote kama chachu njema ya kueneza Injili. Tafakari m.15:Mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe. Kisha wewe mwenyewe pia ushukuru.
Andiko
Kuhusu Mpango huu

Soma Biblia Kila Siku 09/2025 ni mpango mzuri wa kusoma Biblia kila siku sehemu kwa sehemu kwa mwezi Septemba pamoja na maelezo mafupi ya kukusaidia kutafakari somo ulilosoma. Katika mpango huu utasoma zaidi kitabu cha 1 Nyakati na 2 Wakorintho. Karibu kujiunga na mpango huu
More
Tungependa kumshukuru Soma Biblia kwa kutoa mpango huu. Kwa habari zaidi, tafadhali tembelea: www.somabiblia.or.tz
