Siku zilipopita, mkewe bwana wake akamtupia Yosefu macho, akamwambia: Lala kwangu! Lakini akakataa, akamwambia mkewe bwana wake: Tazama! Bwana wangu hajui cho chote kilichomo humu nyumbani, ninachokiangalia, nayo yote, aliyo nayo, ameyatia mkononi mwangu. Humu nyumbani hamna mkubwa kuliko mimi, wala hamna kitu, alichonikataza, ni wewe peke yako, kwa kuwa wewe ndiwe mkewe. Kwa hiyo nitawezaje kufanya kibaya kilicho kikuu kama hiki nikimkosea Mungu?